Our Lady of Medjugorje Messages

Wanangu wapendwa! Pendeni, salini na shuhudieni uwepo wangu kwa ajili ya wale wote walio mbali. Kwa njia ya ushuhuda wenu na mfano wenu mnaweza kuvuta mioyo iliyo mbali na Mungu na neema yake. Mimi nipo pamoja nanyi na kukuombeeni kila mmoja wenu ili kwa upendo na uhodari muweze kushuhudia na kuwahimiza wale wote walio mbali na Moyo wangu usio na doa. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, mitume wa upendo wangu, inawapasa ninyi kuujulisha upendo wa Mwanangu kwa wale wote ambao hawakumjua. Inawapasa ninyi, mianga midogo ya ulimwengu, ambao mimi ninaifunza kwa upendo wa kimama ili ing'ae waziwazi kwa mwangaza kamili. Sala itawasaidia, maana sala huwaokoa ninyi, sala huuokoa ulimwengu. Kwa hiyo, wanangu, salini kwa maneno, kwa moyo, kwa upendo wenye huruma na kwa sadaka. Mwanangu aliwaonyesha njia: Yeye aliyejimwilisha na kunifanya kuwa kalisi ya kwanza; Yeye ambaye kwa sadaka yake isiyo na kifani aliwaonyesha kama inavyopaswa kupenda. Kwa hiyo, wanangu, msiogope kusema kweli. Msiogope kujigeuza wenyewe na ulimwengu ili kueneza mapendo, mkitenda kila jinsi kusudi Mwanangu aweze kujulikana na kupendwa kwa kuwapenda wengine kwa ajili yake. Mimi, kama mama, nipo daima pamoja nanyi. Namwomba Mwanangu awasaidie ili katika maisha yenu upendo utawale: upendo uishio, upendo uvutao, upendo utoao uzima. Huo ndio upendo ninaowafundisha, upendo safi. Inawapasa ninyi, mitume wangu, kuutambua, kuuishi, kuueneza. Waombeeni wachungaji wenu kwa moyo, ili waweze kumshuhudia Mwanangu kwa upendo. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Katika wakati huu wa neema nawaalika nyote kufungua mioyo yenu kwa huruma ya Mungu ili kwa ajili ya sala, toba na maamuzi kwa ajili ya utakatifu muanze maisha mapya. Majira haya ya kuchipua yanawaita, katika mawazo yenu na mioyo yenu, kuishi maisha mapya, kujifanya upya. Kwa hiyo, wanangu, mimi nipo pamoja nanyi niwasaidie ili mkatakati wa kukata shauri muweze kusema NDIYO kwa Mungu na amri za Mungu. Ninyi si peke yenu, mimi nipo pamoja nanyi kwa njia ya neema ambayo Yeye Aliye juu hunijalia kwa ajili yenu na kwa uzao wenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama naja kuwasaidieni kuwa na upendo zaidi, maana yake imani zaidi. Naja kuwasaidieni kuishi kwa upendo maneno ya Mwanangu, ili ulimwengu uwe tofauti. Kwa sababu hiyo nawakusanya, mitume wa mapendo yangu, karibu nami. Niangalieni kwa upendo, ongeeni nami kama vile na Mama kuhusu mateso yenu, maumivu yenu, furaha zenu. Ombeni ili nisali Mwanangu kwa ajili yenu. Mwanangu ni mwenye rehema na haki. Moyo wangu wa kimama ungependa ninyi pia muwe hivyo. Moyo wangu wa kimama ungependa ya kuwa ninyi, mitume wa mapendo yangu, mngeongea kwa maisha yetu juu ya Mwanangu na juu yangu pamoja na watu wote walio karibu nanyi, ili ulimwengu uwe tofauti, ili wairudie imani na tumaini. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini kwa moyo. Salini kwa upendo, salini kwa matendo mema. Salini ili wote wamjue Mwanangu, ili ulimwengu ugeuke, ulimwengu uokoke. Ishini kwa upendo maneno ya Mwanangu. Msihukumu, lakini mpendaneni, ili Moyo wangu uweze kushinda. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Leo nawaalika kuishi kwa kina imani yenu na kumwomba Aliye juu ili aiimarishe, hivyo upepo na dhoruba yasije yakaivunja. Mizizi ya imani yenu iwe sala na tumaini katika uzima wa milele. Tokea sasa, wanangu, jijengeni wenyewe, katika wakati huu wa neema ambapo Mungu anawapeni neema ili kwa njia ya kujinyima na mwito wa kuongoka muwe watu wenye imani na tumaini safi na ya kuvumilia. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, ninyi mnaojaribu kumtolea Mwanangu kila siku ya maisha yenu, ninyi mnaojaribu kuishi pamoja naye, ninyi mnaosali na kujitolea, ninyi ni matumaini katika ulimwengu huu wenye udhia. Ninyi ni miali ya mwanga wa Mwanangu, Injili iliyo hai, na ninyi ni mitume wangu wapenzi wa upendo. Mwanangu ni pamoja nanyi. Vili vile, lakini, Yeye anawangojea kwa uvumilivu wale wasiomjua. Kwa hiyo ninyi, mitume wa upendo wangu, salini kwa moyo na onyesheni kwa matendo upendo wa Mwanangu. Kwenu ninyi hiyo ni matumaini ya pekee, na njia ya pekee kuelekea uzima wa milele. Mimi, kama Mama, ni hapa pamoja nanyi. Sala zenu mnazoniomba ni kwangu mawaridi ya upendo mazuri kuliko yote, Siwezi kutokuwapo pale ninapohisi harufu ya mawaridi. Kuna matumaini! Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Leo nawaalika kusali kwa ajili ya amani. Amani katika mioyo ya wanadamu, amani katika familia na amani duniani. Shetani ana nguvu na anataka ninyi nyote kuwa wapinzani wa Mungu, kuwarudisha katika yote yaliyo ya kibinadamu na kuteketeza katika mioyo yote hisia zinazowaongoza kwa Mungu na mambo ya Mungu. Ninyi, wanangu, salini na mpambane na uyakinifu, shauku ya mambo ya kisasa na ubinafsi ambayo malimwengu huwatolea. Wanangu, kateni shauri ya kuwa watakatifu na mimi, pamoja na Mwanangu Yesu, nitawaombeeni. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Mwanangu alikuwa chemchemi ya upendo na mwanga alipoongea na watu wa mataifa yote. Mitume wangu, fuateni mwanga wake, si rahisi, yawapasa kuwa wadogo, yawapasa kuwa wadogo kuliko wengine wote na kwa msaada wa imani kujazwa na upendo wake. Hakuna mtu duniani, pasipo imani, awezaye kuwa na uzoefu wa mwujiza. Mimi nipo pamoja nanyi, ninajionyesha kwa matokeo hayo, kwa maneno hayo, nataka kuwashuhudia upendo wangu na utunzaji wangu wa kimama. Wanangu, msipoteze wakati mkiweka maswali ambayo hamtapata kamwe majibu, maisha yenu duniani yatakapomalizika Baba wa Mbinguni atawajibu. Mjue daima ya kuwa Mungu hujua yote, Mungu huona, Mungu hupenda. Mwanangu mpenzi sana huangaza maisha na kupasua giza. Upendo wa kimama unaonileta kwenu hauelezeki, umefichwa lakini ni halisi, ninawaonyesheni hisia zangu, upendo, hisani na ukarimu wangu wa kimama. Kutoka kwenu, mitume wangu, ninatafuta sala zenu: mawaridi yaliyo matendo ya upendo, hizo ndizo kwa moyo wangu wa kimama sala za kunipendeza sana, haya ninayaletea Mwanangu aliyezaliwa kwa ajili yenu. Yeye anawatazama ninyi na kuwasikia. Sisi tupo kila siku karibu nanyi kwa upendo wenu ambao huita, huunga, huongoa, hutia moyo na kujaza. Kwa hiyo mitume wangu pendaneni daima, lakini hasa mpende Mwanangu, hii ni njia ya pekee ya wokovu kuelekea uzima wa milele, hiyo ni sala ya kunipendeza ambayo kama harufu nzuri ajabu ya mawaridi, hujaa moyo wangu. Ombeni daima, waombeeni wachungaji wenu ili wapate nguvu ya kuwa mwanga wa Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Kwa furaha kubwa leo nawaletea Mwanangu Yesu ili Yeye awapeni amani Yake. Wanangu, fungueni mioyo yenu na muwe wafurahivu, ili muweze kuipokea. Mbingu ni pamoja nanyi na zinapambana kwa ajili ya amani mioyoni mwenu, katika jamaa na ulimwenguni na ninyi, wanangu, msaidieni kwa sala zenu ili iwe hivyo. Ninawabariki pamoja na Mwanangu Yesu na kuwaomba msikose matumaini, na mtazamo wenu na moyo wenu yaelekee daima mbinguni na uzima wa milele. Hivyo mtafunguliwa kwa Mungu na mipango Yake. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Katika tokeo la mwisho wa kila siku la tarehe 12 Septemba 1998 Mama Maria alimwambia Yakobo ya kuwa ataona tokeo lake mara moja kila mwaka, tarehe 25 Desemba, siku ya Kristmasi. Hivyo ikatokea na mwaka huu. Mama Maria ametokea pamoja na Mtoto Yesu mikononi mwake. Tokeo likaanza saa nane adhuhuri na dakika ishirini na kudumu dakika kumi. Yakobo, baadaye, akatoa ujumbe ufuatao:
Wanangu wapendwa, Leo katika siku hii ya neema nawaalika hasa kusali kwa ajili ya amani. Wanangu, nimekuja hapa kama Malkia wa Amani na mara nyingi nimewaalika kusali kwa ajili ya amani. Lakini wanangu, mioyo yenu imefadhaika. Dhambi inawazuia kufunguliwa kabisa kwa neema na amani ambayo Mungu ataka kuwapeni. Ili kuishi amani, wanangu, yawapasa kuwa kwanza na amani mioyoni mwenu na kujiachia kabisa kwa Mungu na mapenzi Yake. Msitafute amani na furaha katika mambo ya dunia hii maana haya yote hupita. Muelekee rehema ya kweli, amani itokayo kwa Mungu tu na hivyo mioyo wenu hivyo tu itajaa furaha ya kweli; hivyo tu mtaweza kuwa mashahidi wa amani katika dunia hii ya hofu. Mimi ni mama yenu na ninawaombea kila mmoja wenu mbele ya Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`